Wednesday, December 7, 2011

Chelsea yafuzu hatua ya mtoano Ulaya

Andre Villas-Boas amesema Chelsea imewaumbua waliokuwa wakiwabeza baada ya kufuzu hatua ya mtoano ya Ubingwa wa Soka kwa vilabu vya Ulaya kwa ushindi mnono dhidi ya Valencia.
Didier Drogba aifungia Chelsea mabao mawili
Didier Drogba aliifungia Chelsea mabao mawili
Meneja huyo wa Chelsea aliyasema hayo baada ya timu yake kuilaza Valencia mabao 3-0, akiongeza ilikuwa "mateso" kwa klabu yake kwa siku za karibuni kutona na kiwango chao kuporomoka.
"Wachezaji wangu wanastahili heshima ambayo hawapewi," alisema Villas-Boas.
"Tumekuwa tukisumbuliwa na watu mbalimbali tofauti na chagizo zikizidi. Sasa tumewazaba kofi la uso wote hao."

Ushindi huo muhimu wa Chelsea dhidi ya Valencia ulikuwa ni watano katika mechi 11 zilizopita lakini ulitosha kwa timu hiyo kumaliza wakiwa vinara wa kundi E wakifuatiwa na Bayer Leverkusen ya Ujerumani, waliotoka sare na Genk.

Na Villas-Boas alitumia nafasi hiyo kuvishambulia vyombo vya habari kwa namna vilivyokuwa vikitangaza habari za timu yake.

Anahisi vinara wa Ligi Kuu ya England Manchester City hawamo kwenye chagizo kubwa kutoka kwa vyombo vya habari, hata wanapokalia kuti kavu kuelekea kuondolewa hatua ya makundi ya Ubingwa wa Ulaya, walipolazwa na Napoli.

"Natumai Manchester City watafuzu hatua ya mtoano ya Ubingwa wa Ulaya lakini namna vyombo vya habari vilivyokuwa vikiandika kuhusu wao, iwapo watafuzu watakuwa wamefuzu, iwapo hawatafanikiwa kufuzu watakuwa hawajafanikiwa, jambo ambalo vyombo vya habari vilikuwa haviandiki na kutangaza dhidi yetu."
Villas-Boas zaidi hakupendezwa na maoni ya mlinzi wa zamani wa Manchester United na England Gary Neville aliyoyatoa kabla ya mechi yao dhidi ya Valencia.

Nayo Arsenal ililazwa nchini Ugiriki lakini bado imefanikiwa kusonga mbele hatua ya mtoano ya Ubingwa wa Ulaya baada ya kumaliza ikiongoza kundi F.

Mabao yaliyofungwa na Rafik Djebbour, David Fuster na Francois Modesto yaliipatia Olympiakos ushindi wa mabao 3-1- lakini walishindwa kufuzu baada ya Marseille kushinda mchezo wao dhidi ya Dortmund.
Yossi Benayoun aliifungia Arsenal bao hilo moja la kufutia machozi kwa mkwaju wa yadi 15.

Lakini mbali ya kupoteza mchezo huo, usiku ulikuwa mbaya kwa Arsenal baada ya mlinda mlango Lukasz Fabianski na mlinzi wa kushoto Andre Santos walitolewa nje baada ya kuumia.

Haukuwa mchezo mzuri uliooneshwa na Arsenal ambao Wenger angependelea wakati mechi hiyo ya jana alikuwa akitimiza mchezo wa 200 tangu aanze kuisimamia mechi za Ulaya, mechi 44 alipokuwa Monaco na 156 kwa Arsenal.

No comments:

Post a Comment