Showing posts with label Sport. Show all posts
Showing posts with label Sport. Show all posts

Wednesday, December 7, 2011

Santos wa Arsenal nje mechi ya Everton

Mlinzi wa kushoto wa Arsenal Andre Santos, ameondolewa katika kikosi kitakachocheza siku ya Jumamosi dhidi ya Everton katika mfululizo wa mechi za Ligi Kuu ya Kandanda ya England baada ya kuumia kifundo cha mguu wakati wa mchezo na Olympiakos.

Andre Santos aumia kifundo cha mguu hatacheza na Everton
Andre Santos
Santos alilazimika kutoka uwanjani dakika ya 51 siku ya Jumanne baada ya Arsenal kulazwa mabao 3-1 katika mchezo wa mwisho wa kundi lao la F kuwania kufuzu kwa hatua ya mtoano ya Ubingwa wa Ulaya.

Hhc Alive ina habari kuwa Santos, ambaye ameshacheza tangu mwanzo mechi 12 za Arsenal katika mashindano yote msimu huu, huenda akakosa mechi hiyo moja tu dhdi ya Everton.

Walinzi wengine wa pembeni wa Arsenal Carl Jenkinson, Kieran Gibbs na Bacary Sagna nao wagonjwa.

Gibbs anaendelea kupata nafuu baada ya kufanyiwa upasuaji wa mshipa wa ngiri mwezi uliopita na hatazamiwi kucheza mechi na Everton, wakati Jenkinson anakabiliwa na maumivu ya mgongo.

Sagna alivunjika mguu wakati Arsenal ilipolazwa na Tottenham mwezi wa Oktoba.

Wenger huenda akalazimika kumchezesha nafasi ya ulinzi wa kushoto Thomas Vermaelen kutokana na walinzi wa kutumainiwa wa pembeni karibu wote kuumia.

Santos, ambaye amshacheza mechi 22 za kimataifa kwa timu yake ya taifa ya Brazil, alijiunga na the Gunners msimu huu akitokea klabu ya Uturuki ya Fenerbahce kwa kitita cha paundi milioni 6.

Rwanda kumenyana na Sudan nusu fainali

Rwanda itacheza dhidi ya Sudan katika nusu fainali ya Kombe la Cecafa Senior challenge kwa nchi za Afrika mashariki na kati. 

Timu zote mbili zilifuzu kufuatia ushindi katika robo fainali siku ya Jumatatu.
Sudan waliwaondoa Burundi kwa kuwafunga mabao 2-0, ilhali Rwanda ilifuzu baada ya kuishinda Zanzibar mabao 2-1.

Amir Abdelnabi aliifungia Sudan katika kipindi cha kwanza, na bao la pili likafungwa na Musa Mohamed katika kipindi cha pili.

Rwanda ilifanikiwa kuibandua Zanzibar kufuatia bao la ushindi lililofungwa na Meddie Kagere dakika mbili kabla ya mechi kumalizika.

Amavubi walikuwa wameshafunga bao la kutangulia katika dakika ya 39 kupitia Jean Baptiste Mugiraneza, lakini muda mfupi baadaye Abdulrahman Mohammed akaisawazishia Zanzibar.

Robo fainali mbili zinachezwa Jumanne, huku Uganda ikichuana na Zimbabwe, nao wenyeji Tanzania bara wakipambana na Malawi.

Washindi kwenye robo fainali hizo ndio watakaokutana katika nusu fainali ya pili.
Nusu fainali kati ya Rwanda na Sudan itachezwa siku ya Alhamisi.

Chelsea yafuzu hatua ya mtoano Ulaya

Andre Villas-Boas amesema Chelsea imewaumbua waliokuwa wakiwabeza baada ya kufuzu hatua ya mtoano ya Ubingwa wa Soka kwa vilabu vya Ulaya kwa ushindi mnono dhidi ya Valencia.
Didier Drogba aifungia Chelsea mabao mawili
Didier Drogba aliifungia Chelsea mabao mawili
Meneja huyo wa Chelsea aliyasema hayo baada ya timu yake kuilaza Valencia mabao 3-0, akiongeza ilikuwa "mateso" kwa klabu yake kwa siku za karibuni kutona na kiwango chao kuporomoka.
"Wachezaji wangu wanastahili heshima ambayo hawapewi," alisema Villas-Boas.
"Tumekuwa tukisumbuliwa na watu mbalimbali tofauti na chagizo zikizidi. Sasa tumewazaba kofi la uso wote hao."

Ushindi huo muhimu wa Chelsea dhidi ya Valencia ulikuwa ni watano katika mechi 11 zilizopita lakini ulitosha kwa timu hiyo kumaliza wakiwa vinara wa kundi E wakifuatiwa na Bayer Leverkusen ya Ujerumani, waliotoka sare na Genk.

Na Villas-Boas alitumia nafasi hiyo kuvishambulia vyombo vya habari kwa namna vilivyokuwa vikitangaza habari za timu yake.

Anahisi vinara wa Ligi Kuu ya England Manchester City hawamo kwenye chagizo kubwa kutoka kwa vyombo vya habari, hata wanapokalia kuti kavu kuelekea kuondolewa hatua ya makundi ya Ubingwa wa Ulaya, walipolazwa na Napoli.

"Natumai Manchester City watafuzu hatua ya mtoano ya Ubingwa wa Ulaya lakini namna vyombo vya habari vilivyokuwa vikiandika kuhusu wao, iwapo watafuzu watakuwa wamefuzu, iwapo hawatafanikiwa kufuzu watakuwa hawajafanikiwa, jambo ambalo vyombo vya habari vilikuwa haviandiki na kutangaza dhidi yetu."
Villas-Boas zaidi hakupendezwa na maoni ya mlinzi wa zamani wa Manchester United na England Gary Neville aliyoyatoa kabla ya mechi yao dhidi ya Valencia.

Nayo Arsenal ililazwa nchini Ugiriki lakini bado imefanikiwa kusonga mbele hatua ya mtoano ya Ubingwa wa Ulaya baada ya kumaliza ikiongoza kundi F.

Mabao yaliyofungwa na Rafik Djebbour, David Fuster na Francois Modesto yaliipatia Olympiakos ushindi wa mabao 3-1- lakini walishindwa kufuzu baada ya Marseille kushinda mchezo wao dhidi ya Dortmund.
Yossi Benayoun aliifungia Arsenal bao hilo moja la kufutia machozi kwa mkwaju wa yadi 15.

Lakini mbali ya kupoteza mchezo huo, usiku ulikuwa mbaya kwa Arsenal baada ya mlinda mlango Lukasz Fabianski na mlinzi wa kushoto Andre Santos walitolewa nje baada ya kuumia.

Haukuwa mchezo mzuri uliooneshwa na Arsenal ambao Wenger angependelea wakati mechi hiyo ya jana alikuwa akitimiza mchezo wa 200 tangu aanze kuisimamia mechi za Ulaya, mechi 44 alipokuwa Monaco na 156 kwa Arsenal.

Tanzania na Uganda nusu fainali

Kombe la Cecafa
Kombe la Cecafa
Uganda itamenyana na wenyeji Tanzania Bara katika nusu fainali ya Kombe la Cecafa siku ya Alhamisi, baada ya timu zote mbili kushinda katika mechi za robo fainali siku ya Jumanne mjini Dar es salaam.

Uganda Cranes waliishinda Zimbabwe 1-0 katika mechi ya kwanza, nao Kilimanjaro Stars wakawafurahisha mashabiki wa nyumbani kwa kuifunga Malawi 1-0 katika robo fainali ya mwisho.
Bao lao la Tanzania Bara la ushindi lilifungwa na Nurdin Bakari katika dakika ya 35, kwa kukamilisha pasi kutoka Mrisho Ngasa.

Tanzania Bara ndio mabingwa watetezi wa kombe hilo.
Zimbabwe waliudhibiti mchezo dhidi ya Uganda lakini wakakosa bahati ya kufunga.
Hamis Kiiza ndiye aliyefungia Uganda bao hilo moja.
Nusu fainali nyingine siku ya Alhamisi itakuwa kati ya Sudan na Rwanda.